Home » » SERIKALI YATAKIWA KUWEKA BAJETI YA KUONDOA MAGUGUMAJI

SERIKALI YATAKIWA KUWEKA BAJETI YA KUONDOA MAGUGUMAJI

MADIWANI wa halmashauri ya wilaya ya Bunda, mkoani Mara, wameiomba serikali kutenga bajeti kubwa kwa ajili ya kushughulikia suala la Gugumaji katika ziwa Victoria na kwenye mabwawa, kwani yanahatarisha uwepo wa ziwa na mabwawa hayo.

Madiwani hao wameyasema hayo jana kwenye warsha ya kutambulisha na kujenga uelewa kuhusu mradi wa udhibiti wa Gugumaji katika Bonde la ziwa victoria, iliyofanyika katika ukumbi wa halmashauri mjini Bunda.

Wamesema kuwa kwa sasa hivi Gugumaji limevamia sana katika ziwa hilo na kwenye mabwawa, na kwamba kwa hali hiyo ipo haja kwa serikali pamoja na halmahauri ya wilaya ya Bunda, kutenga bajeti kubwa ya kushughulikia hali hiyo.

Aidha, wamesema kuwa bajeti hiyo ambayo itakuwa ni kwa ajili ya kununua mitambo ya kisasa ya kuondoa Gugumaji kwa urahisi zaidi katika ziwa hilo, pamoja na kwenye mabwawa, ambayo yamechimbwa kwa mamilioni yafehda za walipa kodi.

Wamefafanua kuwa katika ziwa victoria Gugumaji yamekuwa mengi sana hususani upande wa wilayani Bunda, na kwamba njia pekee ni kutenga bajeti ambayo pamoja na kununua mitambo ya kisasa itasaidia pia kuajiri vibarua watakaotumia nyenzo rahisi kwa ajili ya kuyaondoa na kudhibiti hali hiyo.

Wamesema kuwa bila kuchukuliwa hatua madhubuti ziwa victoria linaweza likajawa na Gugumaji ambalo linaenea kwa kasi kubwa na kuongeza kuwa pia ziwepo sheria za kuwadhibiti watu wanaovamia vyanzo vya maji.


Mwezeshaji mmoja katika warsha hiyo ambaye pia ni afisa kutoka ofisi ya maji bonde la Musoma na mwanakamati wa mradi wa Gugumaji Bw. Oscar Dimosso, amesema kuwa changamoto ya kudhibiti Gugumaji ni kubwa ikiwemo ya kutokuwepo kwa vitendeakazi vya kutosha.

Dimasso amesema kuwa tatizo jingine ni viongozi kutokusimamia sheria ambapo hali hiyo inachangia kwa kiasi kikubwa uchafuzi wa mazingira, kwa sababu baadhi ya watu hufanya kazi za kibinadamu kwenye vyanzo vya maji.

Awali Doroth Lusheshaniji kutoka ofisi ya huduma ya mimea Mwanza, alisema kuwa malengo ya mradi huo, pamoja na mambo mengine ni kuweka mfumo rahisi wa kupeana habari za udhibiti na ufuatiliaji wa shughuli za Gugumaji.

Mratibu wa mradi huo katika wilaya ya Bunda, Bw. Charles Masawa, amesema kuwa tayari imetengwa bajeti kupitia mradi wa LVEMP, kwa ajili ya kuondoa Gugumaji katika bwawa la Kisangwa lililoko wilayani humo, ambalo sehemu kubwa yake imeshamezwa na mmea huo.

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Mara Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa