Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
IDARA ya Elimu katika Wilaya ya Bunda mkoani Mara, inakabiliwa na
changamoto mbalimbali ikiwamo upungufu wa walimu, migogoro ya mipaka
ya maeneo ya shule, utoro wa wanafunzi na kitengo cha ukaguzi kukosa
chombo cha usafiri.
Hayo yalibainishwa jana katika mkutano wa kuboresha elimu wilayani
hapa, uliofanyika katika Ukumbi wa Chuo cha Ualimu Bunda, mjini hapa.
Ofisa Elimu wa Shule za Msingi wilayani hapa, Jeshi Lupembe, alisema
kuna upungufu wa walimu 236 na kwamba katika mgawo wa walimu wapya,
wamefanikiwa kupata walimu 86, huku wanaostaafu mwaka huu wakiwa 65.
Lupembe alisema changamoto nyingine ni mwamko duni wa wazazi na
walezi kuchangamkia elimu, kwani baadhi yao hawafuatilii mienendo ya
masomo ya watoto wao.
Changamoto nyingine aliitaja kuwa ni ukosefu wa usafiri kwa ajili ya
ukaguzi, kwa sababu gari lililopo ni bovu, kutokuwepo usimamizi wa mara
kwa mara na ukosefu wa chakula cha wanafunzi kwa baadhi ya shule.
Ofisa Elimu wa Shule za Sekondari wilayani hapa, Martin Nkwabi,
alisema changamoto kubwa ni upungufu wa walimu wa masomo ya sayansi,
hali ambayo imekuwa ikisababisha wanafunzi kutokufanya vizuri katika
masomo hayo.
Nkwabi alisema pamoja na kuwa na upungufu wa walimu wa masomo ya
sayansi 158, lakini katika mgawo wa walimu wapya wamefanikiwa kupata
walimu 15 wa somo hilo, na kwamba hadi sasa walioripoti ni wanane.
Alisema changamoto nyingine ni upungufu wa vifaa vya kufundishia na
kujifunzia, ikiwa ni pamoja na vitabu vya maabara na dawa na nyenzo
nyinginezo.
Naibu Mkaguzi Mkuu wa Shule za Msingi wilayani hapa, Anna Ouma,
alisema kitengo hicho kinakabiliwa na changamoto nyingi, ambazo
inatakiwa zipatiwe ufumbuzi haraka ili kuinua kiwango cha elimu.
Chanzo;Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment