Home » » ZAHANATI YA MACHIMWERU INAHUDUMIWA NA NESI MMOJA

ZAHANATI YA MACHIMWERU INAHUDUMIWA NA NESI MMOJA

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 

Zahanati ya kijiji cha Machimweru wilayani Bunda ina nesi mmoja tu anayehudumia wagonjwa wote wa kijiji hicho baada ya mganga aliyekuwapo kwenda masomoni.
Kutokana na hali hiyo zahanati hiyo imekuwa ikifungwa mara kwa mara inapotokea nesi amepatwa na dharura.

Kero hiyo imetolewa na wananchi wa kijiji hicho mbele ya mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa, Wilaya ya Bunda, Boniphace Mwita, anayefanya ziara katika jimbo la Bunda, akikagua ilani ya chama hicho kama inatelekezwa, uhai wa chama pamoja na kusikiliza kero za wananchi.

Kufuatia hali hiyo wananchi hao wakiwamo akina mama wajawazito wanaokwenda kujifungua hulazimika kutafuta huduma ya matibabu kwenye zahanati ya kijiji kingine umbali wa zaidi ya kilomita 10.

Aidha, wananachi hao walisema kuwa watu wanaoathirika ni akina mama wajawazito wanaokwenda kujifungua, pamoja na wagonjwa wenye hali mbaya.
“Kuna nesi mmoja tu, sasa anapopata matatizo ama dharura ya kuitwa wilayani amekuwa akiifunga…sasa hapo ndipo tunapohangaika sana na kutembea umbali mrefu wa kutafuta huduma hiyo,” alisema Valentina John.

Wakizungumza kwa niaba ya wenzao Valentina, Paulina Gatani na Pili Mwita, walimuomba Mjumbe huyo kupeleka kero hiyo kwa serikali ili waweze kuletewa mganga na wauguzi zaidi.

Kwa upande wake nesi wa zahanati hiyo, Nyanjura Masatu, alisema kuwa amekuwa akifanya kazi ya ziada bila kupumzika, kutokana na kuwa peke yake na kulazimika kuifunga wakati anapopata dharura, ikiwamo kupeleka taarifa kwenye kata au wilayani.

Mjumbe huyo alisema kuwa ataifikisha kero hiyo kwa mganga mkuu wa wilaya hiyo, ili aone umuhimu wa kuleta mganga kwenye zahanati hiyo, ikiwa ni pamoja na kuongeza wauguzi wengine zaidi.

Zahanati hiyo pamoja na kuhudumia wagonjwa kutoka katika kijiji hicho, pia hutoa huduma kwa wananchi wengine wa vijiji jirani vikiwamo vya kutoka katika wilaya jirani ya Serengeti.
SOURCE: NIPASHE

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Mara Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa