Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
KUTOKANA na kuibuka kwa wakopeshaji binafsi wanaotoza riba kubwa kwa
watu wanaokopeshwa fedha, wakulima, wafanyabiashara na watumishi wa
serikali Kata ya Neruma, Wilaya ya Bunda, mkoani Mara, wameamua
kuanzisha Chama cha Kuweka Akiba na Kukopa, ili waweze kuondokana na
kero hiyo ya kunyonywa.
Chama hicho chenye makao yake makuu Kijiji cha Kasahunga wilayani
hapa, kinajulikana kwa jina la Neruma Initiative Social Development
Association (Nisa), ambacho kwa sasa kina mtaji wa zaidi ya sh milioni
40.
Aidha, ushirika huo una wanachama 37, ambao ni wakulima, wafugaji,
wafuvi na wafanyakazi wa serikali kutoka katika sekta ya elimu na afya,
waliyoko kijiji cha Kasahunga.
Akitoa taarifa kwenye mkutano mkuu wa mwaka wa chama hicho,
Mwenyekiti wa ushirika huo, Josephat Malima, alisema waliamua kuuanzisha
kutokana na kero hiyo ya kukopeshwa kwa riba kubwa na wakopeshaji hao
binafsi.
Malima, alisema kuwa wakopeshaji hao wamekuwa wakiwakata riba ya zaidi ya asilimia 50 hadi 60 na kwamba huo ni unyonyaji mkubwa.
“Sisi watumishi wa serikali, pamoja na wakulima na wavuvi tuliamua
kuanzisha ushirika huu, ili tuweze kuondokana na kero ya kukopa kwa watu
binafisi ambao hutoza riba kati ya asilimia 50 hadi 60, sasa sisi
tunakupoeshana kwa riba ndogo tu ya asilimia tano,” alisema.
Alisema kuwa tangu walipoanzisha chama hicho Julai 3, 2012, wanachama
wake wamekwishapata mfanikio makubwa, ikiwa ni pamoja na kuchukuwa
mikopo ya masharti nafuu na kuitumia kwa kusomesha watoto wao, kuanzisha
maduka na kununua pikipiki kwa ajili ya kufanyia biashara ya kubeba
abiria (bodaboda).
Awali Katibu wa chama hicho, Charles Tizirukwa, alisema lengo lao
jingine ni kutaka kusaidia watoto wanaoishi katika mazingira hatarishi
zaidi, kwa kuwapatia mahitaji ya kibinadamu, ikiwemo elimu, sanjari na
kutoa mikopo ya masharti nafuu kwa wananchi wengine wa nje na ushirika
huo.
Kwa upande wake, mgeni rasmi katika mkutano huo ambaye alikuwa Ofisa
Tarafa ya Kenkombyo, Peter Jandwa, aliyemwakilisha Mkurugenzi wa shirika
la Zinduka, linalosaidia watoto wanaoishi katika mazingira magumu, Maxi
Madoro, aliwataka wananchi wengine kuiga mfano huo, kwa kuanzisha vyama
vya kuweka akiba na kukopa ili waweze kujiinua kiuchumi na kuondokana
na umasikini
Chanzo;Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment