Home » » RORYA WAIPA HALMASHAURI YAO HATI YENYE SHAKA

RORYA WAIPA HALMASHAURI YAO HATI YENYE SHAKA

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 
 
Unapofika kwenye makao ya Halmashauri ya Wilaya ya Rorya mkoani Mara, utavutiwa na majengo mazuri ya ghorofa na miundombinu yake iliyoboreshwa bila kusahau ngazi nzuri zilizojengwa kwa kuzingatia hali ya mtu.
Kuna ngazi zinazowawezesha wenye ulemavu wa miguu kupanda kwa urahisi wakati wanapokwenda kupata huduma.
Licha ya halmashauri hiyo kuwa na mvuto katika majengo yake, bado iko nyuma kiutendaji, yakiwamo mapato ya ndani kuwa hafifu na kusababisha kushindwa kujiendesha kwa kadri inavyostahili na yote hayo yanadaiwa kuchangiwa na kutokuwepo kwa uhusiano mzuri baina ya viongozi wa kisiasa na watendaji wa halmashauri.
Rorya yenye idadi ya watu 217,176, kati ya hao, wanaume 101,907 na wanawake 115,269. Uchumi wa mkoa huu unategemea zaidi kilimo, uvuvi, mifugo na biashara.
Hata hivyo, kukosekana kwa uhusiano mzuri baina ya watendaji wakiwamo wanasiasa kunadaiwa kuchangia katika kushuka kwa ukusanyaji wa mapato.
Wanasiasa lawamani
Baadhi ya viongozi wakuu wa kisiasa wilayani hapa, wanadaiwa kuwazuia wananchi kulipa ushuru, jambo linalodaiwa kuchangia halmashauri kupata hati yenye shaka kwa mwaka 2012/2013.
Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Ludovick Utouh inaonyesha kuwa tangu kuanzishwa kwa Halmashauri ya Rorya, Julai Mosi 2007 imekuwa ikipata hati zenye shaka ambapo ilipata hati yenye kuridhisha kwa miaka miwili pekee.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, mwaka 2007/2008 ilipata hati inayoridhisha, 2008/2009; 2009/2010 na 2010/2011 ilipata hati zenye shaka. Mwaka 2011/2012 hati inayoridhisha na 2012/2013 imepata hati yenye shaka, jambo ambalo limewaumiza wananchi.
Kikao cha madiwani
Julai 22, 2014 kilifanyika kikao cha Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Rorya cha kujadili hoja za CAG.
Kikao hicho kilichofanyika kwenye Ukumbi wa Soa-Utegi, Mkaguzi wa Hesabu Mkoa wa Mara, Pastory Massawe amesema halmashauri hiyo imepata hati yenye shaka kutokana na kubainika kwa upungufu mwingi.
Masawe anasema anashangazwa kwa halmashauri hiyo kuendelea kupata hati yenye shaka mara kadhaa ambapo ripoti za tangu nyuma zilionyesha upungufu mwingi ambao unajirudia.
Miongoni mwake ni kupatikana kwa nyaraka mbalimbali za fedha za malipo ya ununuzi ambazo hazikuwa na viambatanisho
Pia, uhamisho wa ndani kwa ndani kutoka akaunti moja kwenda nyingine kwa njia ya mikopo ndani ya halmashauri, umesababisha akaunti zilizokopesha kushindwa kutekeleza shughuli zake kama ilivyoidhinishwa na miradi kutokamilika kwa wakati.
Masawe anasema katika usimamizi wa fedha na mapato ya ndani kwa kipindi cha ukaguzi mwaka 2012/2013, halmashauri ilikusanya Sh327,964,125 kutoka katika vyake vya ndani ukilinganisha na bajeti ya vyanzo vya ndani ya Sh1,491,770,000, hivyo kushindwa kukusanya Sh1,163,805,875 sawa na asilimia 78.02.
Aidha, katika ukusanyaji hafifu wa mapato ya ndani ya halmashauri, timu ya ukaguzi ilibaini upungufu unaosababisha ukusanyaji hafifu kutokana na kutosimamia vizuri kazi ya kukusanya mapato..
Mkaguzi huyo anasema sababu nyingine ni zabuni za miradi kutotangazwa kwenye magazeti mbalimbali ili kupima uwezo wa makandarasi kwa kushindanishwa.
Anasema katika ununuzi wa huduma uliofanywa kwa wazabuni ambao hawakuthibitishwa baada ya ukaguzi, ilibainika Sh 70,336,751 kulipwa kwa watoa huduma ambao hawakuthibitishwa. Hivyo menejimenti inatakiwa kuhakikisha inafanya ununuzi kutoka kwa wazabuni waliopitishwa na bodi ya zabuni.
“Kwa kweli, sijafurahishwa na aina hii ya hati! Maana ikipatikana inaonekana mkaguzi haishauri vizuri halmashauri kuhusu mambo yaliyojitokeza kwenye ripoti ambayo yanajirudia, upungufu mkubwa ni kwenye ununuzi na kutopata baadhi ya nyaraka kwa miradi wakati wa ukaguzi, jamani kuweni makini kwenye fedha,”anasema Massawe.
Kauli ya madiwani
Madiwani wa halmashauri hiyo wanasema tatizo la halmashauri yao kupata hati yenye shaka inasababishwa na halmashauri yenyewe kushindwa kuwawajibisha watendaji wanaobainika kuenda kinyume na taratibu za kiutendaji zikiwamo za kutumia fedha vibaya kinyume na taratibu.
Diwani wa Ikoma(CCM), Laurent Adriano anasema: “Halmashauri haitapata hati safi iwapo hatutawachukulia hatua wale wanaobainika kubadilisha matumizi ya fedha, mtendaji anakosea badala ya kufukuzwa kazi anahamishwa kwa nini asishtakiwe!
“Halmashauri haichukui hatua madhubuti kuwapeleka mahakamani wahusika na badala yake wanahamishwa, hali hii itaendeleza matatizo kwa kuwa wahusika hawawajibishwi.”
Naye Diwani wa Kitembe (Chadema), Thomas Patrick anasema kumekuwapo na tatizo la uhusiano mbaya baina ya madiwani na watendaji, jambo linalokwamisha shughuli za kimaendeleo.
Anasema Rorya haitajengeka iwapo watu hawataungana na kushirikiana kuhakikisha Rorya inakua kimaendeleo.
Peter Ayoyi, Diwani wa Mirare anasema: “Hii ni aibu, lini Rorya itapata hati safi kama halmashauri zingine? Yote haya yanasababishwa na malumbano yasiyo na manufaa kati ya baadhi ya viongozi wa siasa na Serikali, tunashindwa kufanya shughuli za maendeleo na matokeo yake tunapata hati chafu,” anasema Ayoyi.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Rorya ambaye pia ni Diwani wa Roche(CCM), Charles Ochele anamtaka mwakilishi wa CAG Mara kumshirikisha iwapo halmashauri haitampatia nyaraka na kuahidi kuwa atashirikina na madiwani kuhakikisha zinapatikana.
Anasema kuna haja ya kuanzishwa kitengo cha kutunza nyaraka zote za halmashauri.
Diwani wa Mkoma (Chadema), Lazaro Kitori anasema halmashauri haijawaboreshea wafanyabiashara maeneo wanayoendesha shughuli za biashara hali inayosababisha baadhi ya watu kugoma kulipa ushuru kwa kuwa mazingira wanayofanyia biashara hayafanyiwi usafi na halmashauri ingawa wamekuwa wakilipa pesa za ushuru.
 chanzo;Mwananchi

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Mara Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa