Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
WANANCHI wilayani Bunda, mkoani Mara, wamelalamikia kitendo cha
madiwani wa wilaya hiyo, kutumia fedha na kuunda tume ya watu watatu,
akiwemo mwenyekiti wa halmashauri hiyo, Joseph Malimbe, kwenda kumuona
Katibu Mkuu kwa ajili ya kusitisha uhamisho wa mganga mkuu wa wilaya
hiyo.
Wakizungumza katika kikao cha Baraza la Madiwani, wananchi hao
walisema kuwa ni matumizi mabaya ya fedha za wananchi kwa viongozi hao
kuamua kwenda mkoani Dodoma kwa ajili ya kusitisha uhamisho wa mtumishi
huyo ambao ulikuwa ni halali kwa mujibu wa sheria.
Walisema kuwa wameshangazwa na kitendo hicho kilichofanywa na viongozi
hao kuamua kuunda tume hiyo wakati uhamisho huo umefanyika kwa mujibu
wa sheria.
Mmoja wa wananchi hao, Ascetic Malagila walisema kuwa baraza hilo
limetumika vibaya fedha za wananchi ambapo inasemekana wametumia zaidi
ya sh milioni sita kwa ajili ya safari hiyo.
“Mganga mkuu Charle Nkombe, aliletewa barua ya uhamisho kutoka
Tamisemi lakini baada ya kupata taarifa hiyo, baraza la madiwani
likiongozwa na mwenyekiti huyo waliupinga na kuunda tume ili waweze
kumuona Katibu Mkuu ili afute uhamisho huo,” alisema.
Alisema kuwa amelazimika kuandika kulalamikia matumizi mabaya ya
fedha hizo ambapo nakala ya barua hiyo ameituma Katibu Mkuu wa Tamisemi,
Afisa Usalama wa taifa wa wilaya hiyo, Mkuu wa Wilaya, Taasisi ya
Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Mbunge wa jimbo la Bunda na
Mwibara, pamoja na madiwani wote wa Halmashauri hiyo.
Malagila alisema kuwa kisheria mwajiri anayo haki ya kumpa uhamisho mtumishi yoyote na kumpeleka popote pale nchini.
Alisema kuwa fedha hizo zimetumika vibaya kwani ni vema zingeelekezwa
katika shughuli za maendeleo hususani, ununuzi wa madawati ili
kuwaepusha watoto kukaa chini.
Akizungumza na Tanzania daima kujibu malalamiko hayo, Mwenyekiti wa
halmashauri hiyo, Malimbe, alisema kuwa hilo ni azimio la baraza la
madiwani na kwamba wananchi hawapo juu ya baraza hilo na wala hawapaswi
kuhoji maamuzi hayo.
“Kwa hiyo wewe na hao wananchi mnapinga maamuzi ya Baraza la madiwani”
alisema na kukata simu na kisha akatuma ujumbe wa simu ya mkononi
akisema, “Mheshimiwa Makongo, kila chombo kina taratibu za kujiendesha.
Siku ya baraza ulikuwepo unajua maamuzi ya baraza ndicho chombo cha
maamuzi ya mwisho”
Chanzo:Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment