Home » » ESTHER BULAYA ATAKA WAZAZI WAWEKEZE KWENYE ELIMU

ESTHER BULAYA ATAKA WAZAZI WAWEKEZE KWENYE ELIMU

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Mheshimiwa Esther Bulaya
MBUNGE wa viti maalum Esther Bulaya (CCM), amewataka wazazi na wananchi kwa ujumla kuwekeza kwenye elimu kwa kuboresha miundombinu na kusomesha watoto wao kwa sababu ndio msingi wa maisha.
Mbunge huyo kijana, aliyasema hayo jana kwenye mahafali ya darasa la saba shule ya Msingi Kunzugu wilayani hapa, hafla iliyokwenda sambamba na harambee ya kuchangia uboreshaji wa miundombinu katika shule hiyo.
Bulaya, ambaye pia alichangia sh milioni moja katika harambee hiyo, alisema ni jukumu la wazazi na wananchi kwa ujumla, kuwekeza kwenye elimu kwa kusomesha watoto wao katika mazingira mazuri, ikiwa ni pamoja kuweka miundombinu mizuri katika shule wanazosoma.
Alisema kuwa yeye kama mwananchi wa Bunda na kiongozi anayependa Wilaya yake, ataendelea kusaidia shule hiyo pale inapowezekana kwa kuchangia chochote atakachokuwa anapata, ili iweze kuwa na ubora unaotakiwa kuliko ilivyo sasa.
“Chochote nitakachokuwa ninapata hata kama ni kidogo, nitakuwa ninakileta ili tuweze kusaidiana nanyi tuweze kuiboresha shule hii ili iondokane na mazingira haya… ni aibu kwa shule yenye umri wa zaidi ya miaka 39 kuwa na mazingira kama haya,” alisema.
Katika hatua nyingine, Mbunge huyo alikubali kuwa mlezi wa shule hiyo baada ya kuombwa na wananchi wa Kijiji cha Kunzugu.
Awali Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Hezron Kimaro, akisoma taarifa, alisema kuwa shule yake inakabiliwa na changamoto nyingi, ikiwemo ya upungufu wa nyumba za walimu, kwani mahitaji ni nyumba 15 lakini zilizopo ni mbili tu.
Alisema kuwa, pia shule hiyo haina ofisi za walimu, ambako hulazimika kutumia chumba cha darasa huku mwalimu mkuu akitumia stoo kama ofisi yake.
Nyingine ni upungufu wa madawati kwani mahitaji ni 302 huku yaliyopo ni 198, matundu ya vyoo kwa wanafunzi na walimu ambako yanahitajika 23.
Katika harambee hiyo, sh 2,646,250 zilipatikana zikiwemo fedha tasilimu na ahadi, mifuko 56 ya saruji, bando moja la mabati na misumari.
C;Tanzania Daimahanzo

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Mara Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa