Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
WAGENI waliomilikishwa mashamba makubwa kwa minajili ya uwekezaji na
badala yake kuyatumia kama vigezo vya kuchukulia mikopo kutoka taasisi
za fedha nchini, watanyang’anywa ardhi hizo na kutimuliwa.
Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi
alisema adhabu hiyo itatolewa pia kwa wamiliki wa ardhi wa Kizungu,
ambao wamekuwa wakiwauzia wageni wenzao ardhi walizopewa kuziendeleza
kwa kilimo, ufugaji au uwekezaji mwingine wenye tija na badala yake
kuyakalia maeneo hayo na baadaye kuyafanyia udalali.
“Na tayari serikali iko mbioni kutaifisha mashamba yasiyopungua kumi
wilayani Babati mkoani Manyara na mengine kadhaa katika Wilaya ya
Bagamoyo mkoani Pwani kutoka kwa wageni ambao ama wameshindwa
kuyaendeleza, au wamebadilisha matumizi yake na hata wale walioamua
kuyauza kwa wawekezaji wengine kinyemela,” alisema Lukuvi.
Alibainisha hayo wakati alipofanya ziara ya kushtukiza katika Ranchi
ya Darakuta iliyopo Kijiji cha Gijameda ndani ya Bonde la Kiiru wilayani
Babati mkoani Manyara. Shamba hilo linamilikiwa na wageni kutoka
Uswisi, Rafael Bapstna na mkewe Rita ambao wanasema walilinunua eneo
hilo tangu mwaka 1985.
Hata hivyo, shamba la Darakuta siyo miongoni mwa maeneo ambayo wizara
ina mpango wa kuyarudisha kwa wananchi, badala yake, Waziri amewaagiza
wamiliki hao kulifanyia marekebisho makubwa eneo hilo wanalotumia kwa
ufugaji wa kibiashara ili liwe na tija zaidi ikiwamo kuongeza ajira kwa
wananchi wa kawaida.
“Kumekuwa na tabia ya raia wa kigeni kuja nchini na kudai wao ni
wawekezaji, kisha kujipatia ardhi ambazo baadaye huzitumia kupata mikopo
kutoka benki zetu hapa nchini,” alibainisha Lukuvi.
Aliongeza kuwa mwekezaji yeyote anayewasili Tanzania ni sharti awe na
mtaji, teknolojia na utaalamu wa kile anachotaka kufanya na siyo atumie
rasilimali zilizomo nchini ili kujipatia fedha kutokana na mikopo.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Babati, Crispin Meela alisema
tayari amekabidhi ripoti maalumu ya masuala ya ardhi kwa waziri yakiwemo
majina ya mashamba makubwa zaidi ya 10 ambayo awali yalikuwa chini ya
wawekezaji wakubwa na sasa yatafutiwa hati miliki zake na kugawiwa kwa
wananchi wa eneo hilo.
Mbunge wa eneo hilo, Jitu Soni alitahadharisha kuwa iwapo wananchi
watapewa mashamba hayo, basi iwepo sheria itakayowazuia kuyauza tena
kinyemela “maana unaweza kuwapa maeneo, baadaye wakarubuniwa na watu
wenye pesa halafu wakayauza tena na kubaki bila kitu.”
CHANZO : HABARI LEO.
0 comments:
Post a Comment