Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
WATUMISHI wa Mahakama wilaya za Tarime na Rorya mkoani Mara,
wametakiwa kufanya kazi kwa kuzingatia sheria na kanuni zilizopo ili
kuwapa haki wananchi wanaofika katika chombo hicho.
Aidha, wametakiwa kuhakikisha wanatoa uamuzi wa mashauri
yanayowafikia kwa wakati na kuhimiza askari wanaopeleleza kesi,
kuharakisha upelelezi ili kuondoa malalamiko.
Hayo yalisemwa na Katibu Tawala wa wilaya Tarime, John Marwa kwa
niaba ya Mkuu wa wilaya hiyo, Glorius Luoga, katika uzinduzi wa Wiki ya
Sheria na Utendaji wa Mahakama nchini, iliyofanyika katika uwanja wa
mpira wa Serengeti, wilayani hapa.
Marwa alisema, “pamoja na mahakama kupewa ridhaa ya kutoa haki kwa
wananchi, kumekuwapo na baadhi ya watumishi wasio waadilifu ambao
wanafanya kazi kwa mazoea kwa kukiuka sheria na taratibu za utumishi wa
umma”. Wanafanya wananchi kukosa imani na vyombo vyao vya mahakama
kutokana na watu wachache kuharibu sifa za mahakama zetu kwa tamaa zao
binafsi, watumishi wa mahakama wanatakiwa kuwa waadilifu kwa kutenda
haki na kujiepusha na vitendo vya rushwa kwani ni aduia wa haki,”
alisema Marwa.
Hakimu Mkazi wa Wilaya, Martha Mpaze aliwaomba wananchi kuona
mahakama kuwa ni chombo huru cha kutoa haki kwa wote bila kujali
itikadi. Aliwataka wananchi kuzitumia mahakama kupata haki.
“Fikeni katika ofisi za mahakama kueleza matatizo yenu, ikiwemo
migogoro na itasikilizwa na kutatuliwa bila kusita na kama kuna tatizo
toeni taarifa kwetu wahusika ili tatizo liweze kushughulikiwa,
tunatarajia kutembelea Shule za Msingi, Sekondari na Magereza kutoa
elimu ya wananchi kutambua huduma zinazotolewa na mahakama na haki zao
za msingi.”
Naye Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Mwanzo Tarime Mjini, Denis Wenje
alisema, siku ya Sheria inayoadhimishwa Februari 4 kila mwaka, inapaswa
kutumiwa na wananchi kufika katika eneo la tukio kupata elimu kuhusu
umuhimu wa mahakama na kujua utaratibu wa kupata haki za kisheria.
CHANZO : HABARI LEO.
0 comments:
Post a Comment