Home » » WARUNDI WALIOTOROKA KENYA KUIBUKIA TARIME.

WARUNDI WALIOTOROKA KENYA KUIBUKIA TARIME.

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.

WAKIMBIZI 48 raia wa Burundi waliokuwa wakiishi katika kambi ya Kakuma iliyopo Nairobi, Kenya, wametoroka katika kambi hiyo na kuingia nchini kupitia mpaka wa Sirari, wilayani Tarime kwa madai ya kunyanyaswa.

Kwa mujibu wa baadhi ya wakimbizi waliohojiwa walidai kutoroka katika kambi hiyo kutokana na kukithiri kwa vitendo vya unyanyasaji kutoka kwa wakimbizi wa Kisomali waliopo katika kambi hiyo na hivyo wameamua kuja nchini kutokana na hali ya amani ya utulivu iliyopo.

Naibu Kamishna wa Uhamiaji, Kituo cha Forodha Sirari, Estomih Urio amethibitisha juu ya uwepo wa wakimbizi hao nchini. Ameliambia gazeti hili kuwa, juzi kundi la wakimbizi wa Burundi 26 liliingia nchini kupitia mpaka wa Sirari na baada ya mahojiano, walijieleza walitoka kambi ya Kakuma, Nairobi lakini wamelazimika kutoroka kutokana na kunyanyaswa na wenzao wa Somalia.
“Kati ya wakimbizi hao, kulikuwa na wanaume wanne, wanawake wanane na watoto 14, tuliwapa chakula na malazi na pia kuwapima afya zao na leo (jana) wengine 22) wameingia hivyo kufanya idadi yao kuwa 48.
“Tumewasiliana na uongozi wa Uhamiaji wa mkoa na makao makuu Dar es Salaam na kufikiwa kwa mwafaka wa kuwasafirisha hadi Mwanza na baadaye wapelekwe kwenye makambi ya Nyarugusu mkoani Kigoma na mengine ambako wanahifadhiwa wakimbizi wa Burundi,” alisema Urio.

Alitumia fursa hiyo kuwaasa wakazi wa mipakani kutoa taarifa wanapoona makundi ya watu wasiowafahamu ili waweze kuhojiwa, kupimwa afya na pia kuchukua hatua nyingine za kiusalama na pia kiafya, ikihofiwa wageni wanaweza kuwa chanzo cha kuibuka kwa magonjwa ya kuambukiza endapo watahama nayo kutoka sehemu mbalimbali na kuingia nayo nchini.
CHANZO: GAZETI LA HABARI LEO.

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Mara Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa