Home » » TANAPA YAKABIDHI MABATI 2800 KUSAIDIA UJENZI WA MAABARA NA ZAHANATI WILAYANI SERENGETI

TANAPA YAKABIDHI MABATI 2800 KUSAIDIA UJENZI WA MAABARA NA ZAHANATI WILAYANI SERENGETI


Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 
 Mbunge wa Jimbo la Serengeti Mhe. Marwa Ryoba (kushoto) akipokea msaada wa mabati kutoka kwa Meneja Ujirani Mwema wa TANAPA Bw. Ahmed Mbugi wilayani Serengeti.


Na Jacquiline Mrisho

Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA) limekabidhi jumla ya mabati 2800 kwa Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti mkoani Mara kusaidia ujenzi wa maabara 15 za shule za sekondari na zahanati zilizo katika Kata mbalimbali za wilaya hiyo.

Akikabidhi msaada huo Meneja ujirani mwema wa Tanapa, Ahmed Mbugi amesema TANAPA imetoa msaada huo kusaidia Maendeleo ya Elimu na Afya katika wilaya hiyo.

“Mabati haya ni msaada ambao tumeutoa kwa Wilaya ya Serengeti ikiwa ni muendelezo wa misaada tunayoitoa kwa jamii hii ili kusaidia shughuli za maendeleo wilayani hapa” alisema Mbugi.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti, Naomi Nnko aliongeza kuwa ujenzi wa maabara hizo kutawawezesha wanafunzi kusoma masomo ya sayansi kwa vitendo, na hivyo kuongeza ufaulu katika shule za sekondari wilayani humo.

Aidha, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya hiyo, Juma Keya alishukuru kwa msaada huo toka TANAPA na kuomba mashirika mengine ndani na nje ya Wilaya ya Serengeti kushirikiana na Halmashauri hiyo kuleta maendeleo katika jamii.

Akizungumza katika hafla hiyo, Mkuu wa wilaya ya Serengeti, Maftah Mohammed  aliliomba shirika hilo kuchangia upatikanaji wa madawati katika shule za msingi na sekondari zilizopo wilayani humo.

Mpaka sasa TANAPA imeisaidia Halmashauri hiyo kwenye ujenzi wa maabara katika Kata ya Natta, uchimbaji wa marambo na ujenzi wa mabweni katika shule za Sekondari.


0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Mara Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa