IMEDAIWA kuwa vitendo vya ukeketaji kwa wanawake na wasichana
unaofanyika katika baadhi ya makabila nchini, huchochea zaidi tamaa ya
kufanya ngono kwa wahusika.
Kwamba ukeketaji unaofanyika katika baadhi ya makabila nchini kwa
lengo la kupunguza tamaa ya ngono, umeshindwa kutekeleza lengo hilo.
Kauli hiyo ilitolewa juzi na Mwezeshaji wa Mradi wa Kutokomeza Ukeketaji kwa njia ya majadiliano awamu ya pili, Nasra Suleiman.
Alisema hayo alipozungumza kwenye semina ya siku moja kuwajengea
uwezo wadau wa mapambano dhidi ya vitendo vya ukeketaji katika kata ya
Sepuka wilayani hapa.
Nasra alisema kuwa tafiti zinaonesha wazi kuwa wanawake na wasichana
waliokeketwa, kwa kiasi kikubwa huwa hawatoshelezwi na wapenzi wao
wakati wa kujamiiana.
Alisema kuwa kutokana na kutotoshelezwa kimapenzi, mwanamke husika
huwa na tamaa ya kusaka wanaume mbalimbali kwa lengo la kumpata
mwanamume atakayekata kiu yake. “Kwa hiyo ukeketaji haupunguzi tamaa ya
ngono bali unachochea zaidi tamaa ya kufanya ngono,” alisisitiza Nasra.
Ofisa Ustawi wa Jamii, Sekretarieti ya Mkoa wa Singida, Shukrani
Mbago alisema kuwa vitendo vya ukeketaji bado vipo ; na kwamba kwa hivi
sasa vinafanywa kwa siri kubwa kukwepa mkono wa sheria.
“Vitendo hivi vya kikatili vinavyodhalilisha utu wa mwanamke
vinaendelezwa zaidi na akinamama wenye umri mkubwa ambao bado wanaamini
kuwa kukeketa ni mila yao hawawezi kuiacha ipotee hivi hivi,” alisema
Mbago.
Alisema ili kuvitokomeza kabisa vitendo hivyo, ni lazima elimu zaidi
iendelee kutolewa na wataalamu pamoja na wadau mbalimbali, wakiwemo
viongozi wa madhehebu ya dini, kuhusiana na madhara yatokanayo na
ukeketaji.
Hata hivyo, wanasemina hao walidai kuwa vitendo vya ukeketaji katika
kata hiyo ya Sepuka, vimepungua kwa kiasi kikubwa baada ya jamii
kuelimishwa juu ya madhara ya ukeketaji na ngariba wengi kufa kutokana
na kuwa na umri mkubwa.
Chanzo Gazeti la Habari Leo
0 comments:
Post a Comment