Home » » Tembo wasababisha njaa wilayani Bunda

Tembo wasababisha njaa wilayani Bunda

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 

Na. Immaculate Makilika- MAELEZO

Wilaya ya Bunda, mkoani Mara iko katika hatari ya kukumbwa  njaa kufuatia tembo kuvamia vijiji mbalimbali na kula mazao yaliyopo mashambani pamoja na yaliyohifadhiwa katika vihenge.

Akizungumza na mwandishi wa habari hii  kwa njia ya simu leo,  Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Mji wa Bunda, mkoani Mara, Bi. Janeth Mayanja alisema kuwa tembo wamekuwa wakivamia mashamba na kula  mazao yaliyohifadhiwa kwenye vihenge katika vijiji  vya Kunzungu, Nyatwali, Tamau, Serengeti, Kinyambwiga, Balili na Mihale kiasi ambacho kinaweza kusababisha njaa katika katika vijiji hivyo.

“Kwa takwimu za mwezi huu tu zaidi ya wakulima 30 mashamba yao yamevamiwa na mazao yao yameliwa na tembo, hivyo ninaiomba Wizara ya Maliasili na Utalii ichukue hatua za haraka kukabiliana na changamoto hii” alisema Bi. Mayanja.

Ameongeza kuwa, mwaka 2012 tembo walivamia vijiji jirani ndani ya Wilaya ya Bunda kwa upande wa kusini wa hifadhi ya Taifa ya Serengeti ambapo waliharibu mazao kadhaa yaliyokuwemo mashambani na kwenye vihenge, hata hivyo taarifa zilipelekwa katika wizara ya Maliasili na Utalii  kwa lengo la kufanya tathimini ili kuwalipa fidia wakulima  walioharibiwa mazao yao, hata hivyo  fidia haikupatikana kwa wakati  kitu ambacho kilisababisha  tatizo la njaa katika maeneo hayo.

Bi. Mayanja ameiomba wizara husika ifanye utafiti wa kina kujua ni kwa nini miaka ya hivi karibuni tembo wamekuwa wakivamia kwa wingi katika vijiji vya wilayani Bunda ikiwa ni katika kupatia ufumbuzi tatizo hilo.

Mazao yaliyoliwa na tembo katika vijiji hivyo  ni pamoja na mihogo, mahindi, mtama na  mpunga.

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Mara Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa