Na. Lilian Lundo – MAELEZO - MARA
Idadi
ya uandikishji wa watoto wenye ulemavu shule ya Msingi Kabarimu ‘B’
iliyoko kata ya Kabarimu, Halmashauri ya Mji Bunda, Mkoani Mara imepanda
kutoka watoto 53 mwaka 2015 mpaka watoto 82 mwaka 2016.
Hayo
yameelezwa leo, Mjini Tarime na Mratibu Elimu wa kata hiyo Josephat
Wambura alipokuwa akitoa tathimini ya maendeleo ya elimu katika kata
yake wakati wa semina ya waratibu elimu kata wa mkoa huo kuhusu
mawasiliano na kushirikishana jitihada zenye mafanikio kwenye elimu.
“Changamoto
kuu ilikuwa ni imani potofu ya wazazi, kuwa watoto wenye ulemavu
hawawezi kupata elimu hali iliyopelekea uandikishaji wa shule za msingi
kwa watoto wenye ulemavu kwa miaka ya nyuma kuwa hafifu ambapo kwa mwaka 2015 watoto 53 ndio walioandikishwa huku watoto wengi wenye ulemavu wakiachwa majumbani,” alifafanua Wambura.
Aliendelea kwa kusema kuwa kupanda kwa kiwango hicho cha uandikishwaji wa watoto wenye ulemavu kumetokana na uanzishwaji wa kamati ya Umoja wa Walimu na Wazazi (UWW) katika shule hiyo ambapo kamati hiyo ilitembelea nyumba hadi nyumba na kutoa elimu kwa wazazi juu ya umuhimu wa elimu kwa mtoto bila kujali ikiwa ana ulemavu au hana ulemavu.
Vile vile kamati hiyo ilianzisha kampeni ya kuhamasisha jamii kuibua watoto wenye ulemavu waliofichwa majumbani. Kampeni hiyo ilifanikiwa na kupelekea jumla ya watoto 82 wenye ulemavu kuandikishwa shule mwaka 2016.
Aidha
ofisi ya Elimu ya halmashauri hiyo iliona jitihada ambazo zimefanywa na
kamati ya UWW hivyo kuiongezea shule hiyo walimu wenye ujuzi wa
kufundisha watoto wenye mahitaji maalum.
Kwa upande wake Mkuu wa Kitengo cha Elimu Maalum shuleni hapo, Mwalimu John Lukiko amesema kwamba kitendo cha kuwaficha watoto wenye ulemavu
majumbani ni moja ya changamoto kubwa iliyokuwepo katika halmashauri
hiyo. Aidha aliipongeza kamati ya UWW kwa juhudi walizozifanya za
kuhakikisha watoto wenye ulemavu wanapata elimu kama ambavyo mtoto asiye
na ulemavu anavyopata elimu.
Kamati
za Umoja wa Walimu na Wazazi (UWW) ni moja ya kitengo katika Mpango wa
Kuinua Ubora wa Elimu Tanzania (Education Quality Improvement
Programme-Tanzania) EQUIP-T unaosimamiwa na Serikali ya Tanzania na
kudhaminiwa na Serikali ya Uingereza. Kamati hizo ziliundwa mwaka 2015
katika shule zote za msingi za Serikli katika mikoa ya Dodoma,
Shinyanga, Simiyu, Tabora, Mara, Kigoma na Lindi. Lengo kuu la
uanzishwaji wa kamati hizo ni kuboresha mfumo wa elimu nchini kwa
kuwashirikisha wazazi na walimu.
0 comments:
Post a Comment