na Ahmed Makongo, Bunda
MKAZI wa Kijiji cha Sanzate wilayani hapa, Megota Samson Feja (40), amehukumiwa kifungo cha miaka 30 jela na kuchapwa viboko 12 baada ya kupatikana na hatia ya kumbaka mwanafunzi wa miaka 12.
Akitoa hukumu hiyo, Hakimu wa Mahakama ya Wilaya ya Bunda, Safina Simfukwe, alisema kuwa ameridhika na ushahidi uliotolewa na upande wa mashitaka ambao umethibitisha pasipo shaka kwamba mtuhumiwa alitenda kosa hilo.
Hakimu Simfukwe alisema anamtia hatiani mtuhumiwa huyo na kumhukumu kifungo cha miaka 30 jela na kuchapwa viboko 12 ili liwe fundisho kwake na kwa watu wengine wenye nia ya kufanya vitendo kama hivyo.
Kabla ya hukumu hiyo, mshitakiwa alipewa nafasi ya kujitetea ambapo aliiomba mahakama impunguzie adhabu kwa vile ana majukumu mengi yanayomkabili. Hata hivyo hakimu Simfukwe aliutupilia mbali utetezi huo na kuamua kumpa adhabu hiyo.
Awali, Mwendesha Mashitaka Mkaguzi Msaidizi wa Polisi, Masoud Mohamed alidai kuwa mtuhumiwa alitenda kosa hilo Mei 22, mwaka huu, majira ya saa 6 mchana, katika Kijiji cha Rakana wilayani Bunda.
Masoud alidai kuwa siku ya tukio, mtoto huyo alikwenda kuchota maji kisimani, ndipo mshitakiwa alipomfuatilia na kumvutia vichakani ambako alimvua nguo na kumbaka.
Aliendelea kudai kuwa, baada ya mtoto huyo kubakwa alipiga kelele za kuomba msaada na wananchi wakafanikiwa kufika katika eneo la tukio na wakamkamata mtuhumiwa kisha kumfikisha polisi.
Chanzo: Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment