Home » » Risasi zinavyotumika kuua raia Tarime

Risasi zinavyotumika kuua raia Tarime

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 

Polisi wakiwa katika Doria

Tarime. Katika Kijiji cha Gomsala, Tarime mkoani Mara yupo Matuma Marwa (22), ambaye hakuwahi kufikiria kwamba siku moja atakuwa mlemavu pamoja na kuwa kila binadamu aliye hai ni mlemavu mtarajiwa.
Marwa alipatwa na ulemavu wa mguu Oktoba 9, mwaka jana, baada ya kupigwa risasi na polisi kwenye paja.
“Tulikuwa tunaelekea shambani, tukasikia milio ya risasi ikielekezwa tuliko sisi, risasi moja ilinipata kwenye paja na tangu wakati ule hadi sasa mguu wangu hauko sawa,” alisema Marwa na kuongeza:
“Kazi yangu ni mkulima, ila kwa sasa nashindwa kulima kwa kuwa mguu bado unauma.”
Marwa ni miongoni mwa watu waliopatwa na madhila yatokanayo na vita ya rasilimali baina ya wananchi na wawekezaji.
Marwa anaishi katika kijiji kilicho kandokando ya mgodi wa dhahabu wa North Mara.
Mgodi wa North Mara unamilikiwa na Kampuni ya African Barrick Gold tangu 2006 ilipoununua kutoka kwa Kampuni ya Placer Dome Tanzania, iliyokuwa ikimilikiwa na Afrika Mashariki Gold Mines.
Taarifa rasmi kutoka katika vijiji vinavyozunguka mgodi huo, zinaonyesha kuwa, mbali na waliojeruhiwa na kupata ulemavu wa kudumu, pia wapo waliopoteza maisha kutokana na kupigwa risasi na polisi wanaolinda usalama katika migodi hiyo.
Matukio hayo na mengine ya unyanyasaji, yanawafanya wakazi wa maeneo haya kuchukulia uwepo wa madini ya dhahabu kama kero kwao na siyo neema au baraka kama ilivyotarajiwa.
Watu 24 wanadaiwa kwamba wamekwisha uawa kwa kupigwa risasi katika matukio, akiwamo mkazi wa Kijiji cha Nyangoto, Ryoba Maseke ambaye alipigwa risasi Julai 12, 2012.
Shangazi wa Maseke, Suzana Mwita anasema, marehemu alikuwa mwanafunzi wa kidato cha nne katika shule ya sekondari ya Mugumu, Serengeti na alifika kijijini kusalimia ndugu zake na hapo ndipo mauti yalipomkuta.
Mwaka huohuo, polisi pia wanadaiwa kwamba walimuua kwa risasi mkazi wa kijiji cha Kewanja, Kibwaba Ghati (23) katika tukio la Novemba 6, wakati wananchi wanaodaiwa kuvamia mgodi, walipokurupushwa na askari wa jeshi hilo.
Mama mzazi wa Ghati, Wankrugati Malembela alisema: “Mwanangu alikuwa akichunga ng’ombe, Polisi walikuwa wakiwakimbiza wavamizi na kupiga risasi ovyo, ndipo risasi mojawapo ilipompata kwenye paji la uso na kufariki pale pale”.
Aliongeza: “Polisi waliuchukua mwili wake na kuupeleka mgodini na kuupiga picha wakisema eti alikutwa huko.”
“Tumekuwa tukifuatilia suala hili polisi lakini wanasisitiza kuwa alikutwa mgodini.Tumekwenda Barrick lakini wanatuzungusha tu,” alisema Malembela.
Polisi wajitetea
Diwani wa Kata ya Kemambo, Wilson Mangure alisema tangu 2011 hadi Januari mwaka huu, watu 69 wameuawa kwa kupigwa risasi na polisi huku mamia wengine wakijeruhiwa.
“Bado tunakusanya taarifa, lakini mauaji bado yanaendelea. Mwaka huu wameuawa watu wanne katika matukio matatu tofauti,” alisema Mangure.
Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Tarime/Rorya, Justus Kamugisha alikiri kuwapo kwa vifo ambavyo alisema vinatokana na mapambano na wavamizi wa mgodi.
Hata hivyo alisema mauaji hayo siyo ya mfululizo. “Hakuna mfululizo wa mauaji…, sisi kazi yetu ni kulinda raia na mali zao na kulinda mwekezaji, hatuko hapa kuua watu. Tunapambana na wavamizi ambao wanaingia mgodini kuiba dhahabu na kuharibu mali,” alisema Kamanda Kamugisha na kuongeza:
“Ungekuja hapa ningekuonyesha jinsi wanavyoharibu… kuna dhana kwa wananchi hapa Tarime kuwa dhahabu iliyoko pale ni yao. Wanavamia mgodi wanapambana na polisi. Wapo baadhi ya polisi waliojeruhiwa vibaya.”
Kwa upande wake Kamishna wa Polisi wa Mafunzo na Operesheni, Paul Chagonja ambaye ameshatembelea eneo hilo mara kadhaa, alisema mauaji yanayotokea yana sababu maalumu:
“Polisi siyo wajinga, waue watu bila sababu, haiwezekani, lazima kuwe na sababu…, huo ni mgogoro wa muda mrefu mno na ninyi waandishi wa habari mnapaswa kuwa wazalendo katika suala hilo,” anasema Chagonja na kuongeza: “Pale kuna watu wakorofi wanaopambana na polisi na kuharibu mali.”
Matukio mengine
Matukio hayo yanaendelea kutokea hadi sasa kwani Januari 6, mwaka huu, mkazi wa Kijiji cha Kewanja, Kimosi Leonard alipigwa risasi mguuni baada ya polisi kuvamia kijiji hicho kwa lengo la kukamata baadhi ya watu.
“Mimi nilikuwa napita na safari zangu tu, nikashangaa watu wanakimbia ovyo. Ndipo nilipojikuta nimepigwa risasi ya mguu,” alisema Leonard ambaye anatembea kwa kuchechemea.
Aliongeza: “Siwezi kwenda kulalamika polisi, maana ukifika huko ndiyo unaongezewa kesi nyingine ya kuvamia mgodi.”
Mwingine ni Weigama Range ambaye alisema watoto wake Fredrick (7) na Happiness (6) wamepata ulemavu baada ya kulipukiwa na mabomu ya machozi yaliyorushwa na polisi.
“Watoto wangu walikuwa wakisoma katika shule ya msingi ya Kewanja. Agosti 23, 2011 polisi walirusha mabomu hapo shuleni na wanafunzi walianza kukimbia ovyo, ndipo mtoto wangu Happiness alianguka na kupoteza fahamu. Hadi leo ana tatizo la kuanguka anguka. Fredrick naye alianguka na kung’oka meno matatu ya mbele,” alisema Weigama na kuongeza:
“Mwaka huu, Kamishna wa Operesheni na Mafunzo wa Jeshi la Polisi, Paul Chagonja alikuja kufanya mkutano hapa kijijini na nilimwonyesha watoto na fomu za polisi na aliahidi kunisaidia, lakini sijapata msaada wowote. Nimejaribu kufuatilia polisi na kwa mbunge wetu, lakini sijapata chochote.”
Mbunge wa Tarime, Nyambari Nyangwine alizungumzia hali ilivyo sasa: “Angalau kwa sasa hali inaendelea kuimarika, kuliko zamani hali ilikuwa mbaya zaidi. Hayo mauaji ni kweli yanatokea na lawama nazipeleka kwa Serikali. Siwalaumu Barrick kwa sababu polisi ndiyo wanaofanya mauaji.”
Uvamizi wa mgodi
Baadhi ya wananchi wanakiri kwamba wamekuwa wakivamia mgodi, lakini wanawakosoa polisi kwa kutumia risasi za moto kuwadhibiti.
Marwa Bina (30) ambaye alikiri kwamba aliwahi kufanya uvamizi, alisema wanalazimika kufanya hivyo kwa kuwa hawana ajira.
“Tunavamia pale ili tupate fedha za kujikimu, ila kwa sasa ulinzi umeimarishwa na hata wakikupiga risasi hupewi fidia,” alisema.
Mwingine ni Joshua Masyaga aliyekuwa mvamizi mgodini hapo ambaye alisema vijana wengi waliamini kwamba watafaidika na madini hayo hata kwa kuyaiba tu.
“Mimi nilikuwa mvamizi baada tu ya kumaliza kidato cha nne 2010. Ni kweli nilipata dhahabu na kuuza lakini ni maisha ya hatari mno. Nimeshuhudia rafiki zangu wengi wakiuawa kwa risasi.
Akifafanua jinsi biashara hiyo inavyofanyika, Masyaga alisema kulikuwa na mawakala wa madini ambao huwasiliana na wafanyakazi wa mgodi wanaotoa kifusi nje.
“Kuna matajiri wanaofanya mpango na wafanyakazi wa ndani na polisi nao hushirikishwa. Mawe yakishamwagwa nje wale matajiri hutuma vijana wao kuokota na wengine huvamia tu. Hao ndiyo hupigwa risasi na polisi,” alisema na kuongeza:
“Mawe yakishapatikana tunayapeleka kwa wasafishaji ambao huyasaga na kuyawekea zebaki ili kupata dhahabu ambayo huchukuliwa na matajiri. Hata hivyo siku hizi ulinzi umeimarishwa mno, hiyo biashara imekufa.”
 
Majibu ya Barrick
Meneja wa Mgodi wa North Mara, Gary Chapman alisema:
“Mara nyingi watu wanaouawa ni wale wanaopambana na polisi, vinginevyo tuna uhusiano ni mzuri na wanajamii na ndiyo maana tunafanya nao mikutano kujadili maendeleo na watu wanashukuru kwa huduma zetu.”
Aliongeza: “Kuna watu wanaovamia mgodi wetu. Kwa hiyo unapozungumzia migogoro kama hiyo, siyo kwa mgodi tu bali katika jumuiya nzima.”
Naye Ofisa Uhusiano na Mawasiliano ya Umma wa ABG, Nector Foya alisema kampuni hiyo inao mfuko wa maendeleo (The ABG Maendeleo Fund) ambao hutoa huduma kwa wanajamii wanaozunguka migodi yao.
“Tuna mfuko wa maendeleo ya jamii ambao unasaidia huduma kama vile elimu, maji na afya. Tumejenga shule, hospitali na miradi ya maji katika vijiji vinavyozunguka migodi yetu, ndiyo maana tunasema tunao uhusiano mzuri na wanajamii,” alisema.
Halmashauri Tarime
Wakati kukiwa na matukio yanayozua mvutano baina ya wawekezaji na wananchi, uongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Tarime unajivuna kwa kupata faida kutoka kwenye mgodi huo.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, Athuman Akalamu alisema tangu kampuni ya ABG ilipofika imekuwa ikijitanua, hivyo kuchukua maeneo ya vijiji vilivyo jirani, hali inayosababisha migogoro ya ardhi miongoni mwa wanavijiji kutokana na fidia iliyokuwa ikilipwa.
Alisema kutokana na migogoro hiyo, Serikali iliunda kikosi kazi kwa ajili ya kushughulikia malalamiko husika.
Kiongozi wa kikosi hicho Minja Jeremiah alisema: “Mwaka 2012 Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Steven Masele na aliyekuwa Naibu Waziri wa Ofisi ya Makamu wa Rais, Charles Kitwanga walitembelea mgodi huu baada ya kampuni ya ABG kulalamika kuwa eneo lao halitoshi. Hivyo tathmini ilifanywa na kijiji cha Nyangoto kilitakiwa kutoa eneo”.
Hata hivyo alisema kutokana na hali hiyo, kuliibuka makundi matano ya watu.
“Kundi la kwanza lilipinga kabisa mpango huo, huku la pili likikubali ila kwa kulipwa kwanza fidia, la tatu lilikubali fidia lakini waliendeleza makazi yao, wengine wakakubali sehemu ya fidia na wengine walichukua fidia lakini hawakuhama.
Ndiyo maana kikosi hiki kiliundwa Aprili 2013,” alisema. Alisema tangu wakati huo, wameshafanya uthamini katika vijiji vya Kewanja na Nyakunguru na wanavijiji wameshapata kibali cha Mthamini Mkuu wa Serikali na wamelipwa fidia katika awamu nne.
Hata hivyo anasema wapo watu wapatao 4,000 waliofanyiwa tathmini lakini bado hawajalipwa.
Utatuzi wa migogoro
Katika kurejesha uhusiano mwema kati ya mgodi huo na wanajamii, Shirika la Search for Common Ground lenye makao yake makuu Dar es Salaam, sasa limejikita wilayani Tarime ili kutafuta suluhu.
Meneja Programuwa shirika hilo, Patricia Loreskar alisema kazi kubwa ya shirika hilo ni kujenga mazingira ya mawasiliano na mijadala kwenye mazingira yenye migogoro.
Naye Meneja wa mradi wilayani Tarime, Jacob Malikuza alisema njia wanazotumia ni pamoja na kufanya utafiti wa maisha ya wanajamii kabla ya kuanza kutoa mafunzo.
Kwa upande wake Mwanasheria wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Harold Sungusia anasema wamekuwa wakifuatilia mgogoro katika eneo hilo na wamefungua kesi London, Uingereza ili kuishitaki African Barrick Gold kwa ukiukwaji wa haki za binadamu.
Taarifa zaidi zinaonyesha pia kampuni ya uwakili ya Leigh Day nayo inahusika katika kesi hiyo ikiwawakilisha baadhi ya wanavijiji wanaozunguka mgodi huo, kutokana na matumizi ya nguvu kupita kiasi.
Kesi hiyo iliyofunguliwa mwishoni mwa mwaka jana, ilipingwa na ABG wakitaka iendeshwe Tanzania, lakini walishindwa katika pingamizi lao.
“Huo mgogoro tumeufuatilia sana, hadi sasa tumeshafungua kesi Uingereza.Hatukufungulia Tanzania kwa sababu mahakama zetu zinachelewesha mno kesi na mara nyingine hazitufikishi kwenye kupata haki,” alisema Sungusia.
Hata hivyo Amani Mustafa ambaye ni mwanzilishi na Mkurugenzi wa taasisi ya Haki Madini alisema ni watu wachache mno wenye uelewa na masuala ya sheria hadi kufikia kufungua kesi.
“Watu wachache sana wanaweza kupeleka kesi mahakamani. Kwanza kuna mazingira ya kutishana na kutokuaminiana. Isitoshe wengi hawaoni kama mahakama ndiyo suluhisho la mambo yao. Kwa kifupi wamepoteza imani na Serikali na mfumo mzima wa mahakama. Wanachoamini haki inapatikana mikononi mwao,” alisema Mustafa na kuongeza:
“Kuna mambo mengi mno kwenye mgodi ule; mauaji, unyanyasaji wa kijinsia, uchafuzi wa maji, kutofuatwa kwa taratibu za kazi mgodini na hata vyama vya wafanyakazi vinalalamika”.
Akizungumzia mfumo wa kushughulikia malalamiko, Mustafa alisema kutoelimika kwa wanavijiji ndiyo sababu kubwa ya kukosa haki.
“Kungetakiwa kutolewe elimu ya sheria kwa wanavijiji na mwelimishaji asilipwe na Barrick. Kwa sasa kuna ukiukwaji wa maadili na Serikali haina muda, bali imejikita kwenye ukusanyaji wa kodi kuliko kuangalia haki za watu,” alisema Mustafa.
Chanzo;Mwananchi

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Mara Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa