Home » » Tumuenzi Baba wa Taifa kwa kutumia Kiswahili katika kuitangaza nchi yetu.

Tumuenzi Baba wa Taifa kwa kutumia Kiswahili katika kuitangaza nchi yetu.


Tumuenzi Baba wa Taifa kwa kutumia Kiswahili katika kuitangaza nchi yetu.
Na Shamimu Nyaki-WHUSM
“Mkataa kwao ni mtumwa”ni msemo ambao una maana kwamba binadamu ni lazima ujikubali katika kila hali ambayo unakutana nayo katika mazingira yoyote yale na usikubali binaadamu mwingine akakutawala au akabadilisha mtazamo wako kwa manufaa yake bali kubali kupokea mawazo yanayoweza kuboresha kile unachokiamini.
 Na ndivyo  alivyofanya Baba wa Taifa letu Mwalimu Julius Kambarage Nyerere katika kutumia Kiswahili kama utambulisho wa Mtanzania popote pale atakapokuwa.
 Katika Historia Lugha ya Kiswahili ilianza takriban miaka 800-1000  iliyopita  katika mazingira ya Vituo vya Biashara Ukanda wa Pwani ambako Wafanyabiashara kutoka Uarabuni, Uajemi na Uhindi walikutana na wenyeji Waafrika.
Lugha kuu ya Kimataifa ya Biashara wakati huo ikiwa ni Kiarabu ambapo  kutokana na muingiliano wa watu lugha mpya ilijitokeza wakati wenyeji wa Pwani waliokuwa wasemaji wa Lugha za Kibantu walipopokea maneno mengi hasa ya Kiarabu katika mawasiliano yao.
 Kiswahili kilikuwa na lahaja nyingi kutokana na lugha mbalimbali za Kibantu zilizochangia matumizi  tangu Karne ya 19 ambapo  Kiswahili  kilianza kuenea Barani Afrika kwa njia ya Biashara.
Ni katika kipindi hiki ambapo Mwalimu  Nyerere alikuwa katika harakati za kudai Uhuru wa Tanganyika ndipo alipoamua kutumia lugha ya Kiswahili  kama chombo muhimu cha  kuwaunganisha  watanzania wote  kupigania na kudai  Uhuru.
 Mara baada ya Uhuru mwaka 1961, Kiswahili kilitangazwa kuwa Lugha ya Taifa. Ambapo  Waziri Mkuu wa kwanza wakati ule aliagiza kuwa Kiswahili kitumike katika shughuli zote za Umma.
Na katika kutekeleza  Agizo hilo, tarehe 10 Desemba 1962, Rais wa Tanganyika wakati huo  akiwa Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere alitoa Hotuba ya Jamhuri kwa Lugha ya Kiswahili. Katika utetezi huo, hatua ya kwanza ya Mwalimu Nyerere ilikuwa ni usisitizaji wa matumizi ya Kiswahili kama lugha asilia ambayo raia wa Tanganyika walipaswa kutumia ili kuelewana ifaavyo, na kuondoa uwezekano wowote wa mafarakano yanayohusiana na mitafaruku ya kimatamshi.
Na kwa kuweka mfano wa hatua hiyo, Rais Nyerere alihutubia katika hafla zote rasmi kwa lugha ya Kiswahili, hivyo basi kuhakikisha kuwa kila raia wa Tanganyika; aliyekuwa na kisomo au la; alimwelewa, pamoja na mikakati ambayo Serikali yake ilipaswa kuweka.
La kutia moyo ni kuwa,karibu asilimia 95 ya wakazi asilia wa Tanganyika, ni wenye asili ya Kibantu, hivyo mazingira ya usisitizaji wa uzingatiaji wa Kiswahili kuwa lugha unganishi ya jamii hizo yalifaa.
Hatua ya pili kwa Rais Nyerere ilikuwa ni upitishaji wa Azimio la Arusha la 1967, aliposema kuwa, “ni mfumo wa 'Ujamaa’ pekee ambao ungefikia lengo kuu la uuganishaji wa Watanzania wote”.
Katika hotuba yake, kiongozi huyo alisisitiza kuwa, ni kupitia kwa Ujamaa pekee, ambapo Waafrika wangeweza kupambana na falsafa kandamizi za kibepari, akiurejelea mfumo wa ujima, ambao unawiana moja kwa moja na ujamaa endelevu.
Mwalimu Nyerere pia alikwepa matumizi ya falsafa ya kikomunisti, hasa kutoka mataifa ya Urusi na Uchina, kwani yalihusishwa na ukandamizaji wa haki za binadamu.Badala yake, alisisitiza mfumo wa demokrasia asilia, uliotambua ushiriki wa kila mwanakijijji bila shaka, mafanikio ya ujamaa yaliendelea kujitokeza kwani kadri vijiji hivyo vilivyoendelea kukua, kiwango cha elimu kiliendelea kuimarika nchini Tanzania.
Kwa mfano, kwa wakati mmoja, Tanzania iliorodheshwa nchi iliyokuwa na kiwango kikubwa cha kisomo barani Afrika (asilimia 83) pamoja na mafanikio makubwa katika sekta ya afya.
Hili liliashiria kuwa, hakujikita pekee katika uongozi wa kisiasa, lakini katika utetezi wa Kiswahili, kwani baadhi ya vitabu vyake  aliviandika kwa Kiswahili ili kuwafaa wananchi na kuwafungua macho Watanzania kuhusu ilikokuwa ikielekea nchi yao.
Kutokana na mchango huo, ni wajibu wa viongozi wetu wa kisiasa kutambua kwamba mchango wao katika kuitetea lugha ndiyo utakaowafanya kukumbukwa na vizazi vijavyo.
Uzalendo wa Mwalimu Nyerere unapaswa kuwa mwanga kwa viongozi wote wa Kiafrika kufahamu kwamba kutumia Kiswahili ni wino wa kuandika historia.
Mwalimu Nyerere atakumbukwa kwa kuwa miongoni mwa Waafrika wa kwanza kutafsiri kazi za Kiingereza kwa Kiswahili.
Juhudi hizo zimeendelea kuonekana kwani Januari 1967 Agizo jingine lilitolewa na Makamu wa Pili wa Rais wakati huo Mheshimiwa Rashidi Mfaume Kawawa kwamba, Kiswahili kitumike katika shughuli zote za Kiserikali na Kitaifa.
Kuanzia  hapo Kiswahili kikawa kinatumika katika shughuli zote za Nyanja zote hapa nchini  na kimeimarisha mahusiano ya  makabila na kuifanya Nchi ionekane kama ina  kabila  moja badala ya makabila takriban 120. Kiswahili kimekuwa Nguzo Imara ya Mshikamano, Amani, Utulivu na Upendo miongoni mwa Watanzania.
Ama kwa hakika juhudi hizi zimezaa matunda kwa Watanzania kutokana na umoja uliotakana na juhudi za mwalimu katika kueneza matumizi ya lugha yetu na ni kutokana na juhudi za  viongozi wote wa nchi hii wanavyohimiza  kutumia  lugha hii.
Kudhihirisha hilo Rais wa Awamu ya Nne Dkt. Jakaya Kikwete  katika  hotuba yake kwanza aliyoitoa Bungeni baada ya kuchaguliwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Disemba 2005 alisemaLugha ya Kiswahili imeanza kupata umaarufu Afrika na duniani”.
Umoja wa Afrika umekubali Kiswahili kuwa moja ya lugha zake kuu. Aidha Nchi za Kanda ya Maziwa Makuu zimekubali kutumia na kuendeleza lugha ya Kiswahili.
 “Serikali ya Awamu ya Nne itahakikisha kuwa juhudi hizi zinaendelezwa na kuhakikisha kuwa lugha ya Kiswahili inakua nje ya mipaka ya Afrika”.Alisema Mhe. Kikwete.
Hizi ni jitahada kubwa sana zilizofanywa na ambazo zinaendelea kufanywa na Serikali katika kuhakikisha lugha ya Kiswahili inakuwa kwa kiasi kikubwa.
Kipo chombo Muhimu kilichopewa dhamana ya kuendeleza na kukuza lugha hii kwa ubora zaidi ambacho ni Baraza la Kiswahili la Taifa (BAKITA) ambalo lipo chini ya Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na  Michezo liliundwa chini ya sheria namba 27 ya Bunge ya mwaka 1967 kukuza na kuendeleza matumizi ya Lugha ya Kiswahili katika Tanzania,kushirikiana na taasisi nyingine  ndani ya Jamhuri ya Muungano ambazo zinahusika na kukuza Kiswahili na kuratibu kazi zao,kukuhamasisha matumizi ya Lugha ya Kiswahili katika shughuli rasmi na za umma.
Mafanikio haya ya matumizi ya Kiswahili yamesaidia sana kukuza na kuendeleza lugha ya Kiswahili kwani Hata Rais wa Awamu ya Tano Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli yupo mstari wa mbele katika kutumia lugha hii ya Kiswahili katika hotuba zake na dhifa mbalimbali za Kitaifa Mfano ni wakati alipokutana na Waziri Mkuu wa India Mhe.Narendra Modi tarehe 29 mwezi Agosti 2016.
Watanzania wote tunapaswa kujivunia juhudi hizi na tuwe mstari wa mbele kuendelea kukitumia Kiswahili kama utambulisho wetu ili kueneza utamaduni wa nchi yetu.
MWISHO.


 









1 comments:

Unknown said...

Makala nzuri yenye kuelezea kwa kina juu ya usuli wa maendeleo ya Kiswahili chini ya uongozi shupavu wa hayati mwalimu Nyerere.Kwa kweli tunapaswa kuienzi lugha hii adimu ya Kiswahili.Pia ,ikumbukwe kuwa mwaka 2013 ulikuwa mwaka pekee kwa kiongozi wetu kuenziwa katika umoja wa mataifa(UN).Viongozi wetu hawanabudi kutilia maanani utumizi sahihi wa Kiswahili

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Mara Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa