Home » » KISABABISHI KANSA KISICHO CHA LADHA, HARUFU, RANGI

KISABABISHI KANSA KISICHO CHA LADHA, HARUFU, RANGI

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.


JIFUNZE, uelimike. Je, katika maisha yako umekutana na msamiati wa kisayansi unaoitwa sumu kuvu? Wataalamu wanainisho lake.

Hiyo inatajwa kuwa aina ya kemikali za sumu zinazozalishwa na aina ya ukungu au fangasi wanaoota kwenye mbegu za nafaka, ikiwamo mahindi, karanga, kunde na mazao jamii ya mizizi.
Inaelezwa kuwa asilimia 6O ya watu ambao wamekula sumu kuvu walau kwa kiwango kidogo, lakini katika muda mrefu inawafanya mwili wao kudumaa, kudhoofika na hata baadhi wanapatwa na kansa ya ini.
Aidha, katika kundi la waliokula chakula au nafaka kilichoathiriwa na sumu hiyo kwa kiwango kikubwa, wanaweza kupoteza maisha muda mfupi baada ya kula.
Hayo yamo katika uchambuzi kitaalamu ulioainishwa na mtaalamu wa masuala ya mimea kutoka taasisi ya Kimataifa ya Kilimo cha Kitropiki (IITA), George Mahuku.
Ni ufafanuzi uliotolewa, wakati akitoa elimu ya namna ya kukabiliana na madhara hayo.
Anasema sumu hiyo, pia inaweza kupatikana katika bidhaa za mifugo kama vile maziwa, mayai na nyama, iwapo mnyama au mfugo husika atakuwa amekula chakula kilichoathiriwa na sumu kuvu.
Mahuku anasema barani Afrika, idadi ya watu wanaougua kansa inaongezeka kwa kasi, kutokana na kwamba wana elimu duni kuhusu namna bora ya kuhifadhi mazao.
Pia, anataja mabadiliko ya tabianchi yanayosababisha mimea kukua kwa shida.
Mahuku anasema, sumu kuvu iko katika hali ya kujificha, kwani haionekani kwa macho, haina harufu, ladha, wala rangi.
Mtaalamu wa serikali
Ofisa Mfawidhi anayehusika na Visumbufu Vamizi, kutoka Wizara ya Kilimo, Ufugaji na Uvuvi, Beatrice Pallangyo, anataja msimamo wa serikali kwamba, imeruhusu matumizi ya teknolojia ya kulinda mazao shambani, dhidi ya sumu kuvu.
Anasema teknolojia hiyo itasaidia kupunguza athari hizo, kwa kuwa mazao yanayolimwa katika maeneo yenye ukame, itasaidia kustahimili hali hiyo na kuwa imara.
Beatrice anasema kuwa, serikali inatarajia kusajili teknolojia mpya ya kukabiliana na ugonjwa wa sumu kuvu, ambao unashambulia mazao hususan mahindi na karanga.
Anasema ukaguzi wa ubora wa chakula unafanywa na Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA), kuchukua sampuli kidogo kwa ajili ya kukagua kiwango cha sumu kuvu kama kipimo katika mazao ya nafaka hata zilizopo viwandani.
“Kabla ya kusafirisha nje au mazao yanayoingia nchini hukaguliwa, ili kubaini iwapo kuna sumu hiyo,” anasema Pallangyo.
Pia, anasema ili kuhakikisha mazao yanahifadhiwa na kuwa salama, serikali ilianzisha mfumo wa stakabadhi ghalani, ili kuhakikisha mazao yanahifadhiwa kitaalamu.
Beatrice anasema serikali bado inaendelea kuelimisha jamii kuhusu uhifadhi wa mazao na kuendeleza ushirikiano kati yake na wadau, ili kukabiliana na vita vya kuondoa sumu hiyo katika lishe ya jamii.
Watoto hatarini
Beatrice anasema kwamba watoto walio chini ya miaka mitano ambao wameachishwa kunyonya maziwa ya mama zao, wana hatari zaidi ya kuathiriwa na sumu kuvu.
Anasema familia nyingi baada ya kumwachisha mtoto kunyonya, wanawapa watoto wao uji wa lishe ambao ama wananunua dukani au wanaandaa wenyewe na kwenda kusaga kwenye mashine zinazotoa huduma kibiashara.
“Watoto wetu tunawapa uji uliosagwa, uwe ni wa mahindi, au uliochanganywa na ulezi, mtama, karanga ili kupata lishe. Lakini, tusipozingatia ubora wa nafaka hizo na kama zimepatwa na fangasi wasababishao sumu kuvu tunawahatarishia watoto afya,” anasema.
Anaeleza kuwa fangasi wanaosababisha sumu kuvu, hushambulia mazao yakiwa shambani na hata baada ya kuvunwa na kutokana na kutohifadhiwa vizuri na kusababisha unyevunyevu katika zao.
Beatrice anasema malezi ya watoto wenye umri chini ya miaka mitano nchini hufanana na kwamba wazazi wengi baada ya kuwaachisha kunyonya, hutumia uji wa lishe ya nafaka, kutoka dukani au wanatengeneza wenyewe.
"Uhifadhi wa mazao baada ya kuvuna ukiwa si sahihi na sehemu ukiwa na unyevunyevu huweza kusababisha fangasi wa sumu kuvu, ingawaje vipimo vya kitaalamu vinahitajika kuthibitisha," anasema Beatrice.
Anatahadharisha kuwa, jamii haitakiwi kuhofu suala hilo la sumu kuvu, lakini bado kuna umuhimu mkubwa wa kuelimishwa kwamba kuna tatizo kubwa na hasa kwenye mikoa yenye ukame, ikiwamo Dodoma na Singida.
Udhibiti wake
Mahuku anasema kuwa, sumu kuvu inaweza kudhibitiwa kwa kuhakikisha shamba halishambuliwi na magugu pamoja na wadudu waharibifu.
Pia, anasema inashauriwa kitaalamu kwamba mazao yavunwe katika wakati mwafaka, ambao ni kiangazi na kamwe yasianikwe kwenye udongo.
Anataja njia sahihi ni kuanika mazao kwa kutumia turubai au viroba na mazao hayo yachambuliwe, ili kuondoa mbegu zilizooza shambani au kuharibiwa na wadudu.
“Teknolojia na mbegu bora zinazostahimili changamoto za hali ya hewa zitapunguza tatizo hilo. Usindikaji wa mazao na uhifadhi bora, pamoja na elimu kwa wakulima iongezwe,” anasema.
Anabainisha kuwa, ghala la kuhifadhia chakula, ni lazima liwe na hewa mzunguko na dawa zilizoruhusiwa kibaiolojia, zinaweza kutumika na baadhi yake zina nguvu ya kukinzana na sumu kuvu.

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Mara Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa